Ladda ner PDF
Tillbaka till listan med berättelser

Kuja Norwei

Skriven av Aamiina

Illustrerad av Julie Cornelia van Walsum

Översatt av Jacob Haule

Uppläst av Idrisa Mbaraka

Språk swahili

Nivå Nivå 5

Läs hela berättelsen

Reading speed

Automatisk avspälning


Mimi na kaka zangu wawili tulikuja Norwei mwezi Disemba 2016. Tulivaa nguo za majira ya joto kwa sababu tulifikiri Norwei kutakuwa na joto kama Somalia. Hata hivyo, tulipofika uwanja wa ndege kulikuwa na theluji. Tulihisi baridi na hali ya hewa ilikuwa ya baridi sana. Ingawa tulibeba mabegi, yalikuwa na nguo za majira ya joto tu.


Hata kama kulikuwa na baridi, nilifurahi sana tulipokuja Norwei. Hatimaye niliweza kufanikiwa kuonana tena na mama yangu ambaye sikumuona kwa miaka sita. Tulionana na mama pamoja na rafiki zake wawili. Tulipomuona tulilia kwa furaha. Tulienda kwenye mji mdogo ambapo mama anaishi.


Siku za mwanzo tukiwa katika mji wa mama zilikuwa ni za kustaajabisha. Kulikuwa na baridi na theluji na hatukuweza kuona chochote. Mitaa ilikuwa tupu kabisa. Watu wachache niliokutana nao walionekana wakihisi baridi na hawakuwa sawa. Somalia kulikuwa na watu kila mahali, kwa hiyo kila kitu kilikuwa kigeni hapa. Mama yangu na rafiki zake walitupatia zawadi na kisha akatupeleka kununua nguo za majira ya baridi.


Baada ya mapumziko ya Krismasi, nilijiunga na kozi ya Kinorwei katika kituo cha elimu ya watu wazima. Nilisoma pale kwa muda wa miaka miwili kabla ya kuanza shule ya msingi. Sasa nipo mwaka wa mwisho na nimejitengenezea marafiki wengi. Ninapenda sana kuongea na watu na kufurahia kuonana na watu wapya.


Baada ya masomo, huwa ninaenda kwenye kituo kinachoendeshwa na wajitoleaji ambapo huwa ninasaidiwa kufanya kazi ya nyumbani. Pia nimejiunga na kozi ya kushona katika kituo hiki.


Nilipokuwa Somalia, sikuwahi kwenda shule au kujiunga na kozi yoyote isipokuwa shule ya Kuran. Sikujua kusoma wala kuandika. Sasa nimeshajifunza namna ya kuandika Kisomali na Kinorwei na masomo mengine mengi. Bila elimu, nilijihisi si kitu. Sasa ninajiona mwenye maarifa na furaha.


Mwaka ujao, nitaanza shule ya sekondari katika idara ya afya na maendeleo ya vijana. Hapo baadaye, ninataka kuwatumikia vijana. Nikimaliza elimu yangu, ndoto yangu ni kupata ajira ya kudumu. Pia ninataka kujifunza udereva na nipate leseni yangu ya udereva.


Kama ningebaki Somalia, ninadhani ningekuwa mama mpaka sasa. Pengine ningekuwa na watoto wengi. Kama ningekuwa Somalia, nisingekuwa na fursa sawa kama nilizozipata mpaka sasa. Ninajihisi mwenye bahati kuishi Norwei.


Skriven av: Aamiina
Illustrerad av: Julie Cornelia van Walsum
Översatt av: Jacob Haule
Uppläst av: Idrisa Mbaraka
Språk: swahili
Nivå: Nivå 5
Creative Commons Licens
Detta verk är licensierat under en Creative Commons Erkännande 4.0 Internationell Licens.
Valmöjligheter
Tillbaka till listan med berättelser Ladda ner PDF